Tatizo la usafiri na hali ya hewa vimetufanya tutembelee Shule ya Msingi Bunju 'A', na Shule ya Msingi Kiluvya pekee.
Pale Bunju A tulipokelewa na mwalimu Nzava, mwalimu kijana, mchangamfu, ambaye mara baada ya kueleza kilichotupeleka alitutambulisha kwa mwalimu mkuu msaidizi na walimu wengine (Mwalimu mkuu hakuwepo). Kisha tukapewa nafasi ya kupita madarasani kuongea na wanafunzi na kuwaelekeza kuhusu shindano letu. Vijana walifurahia sana, wakasikiliza kwa makini na kuuliza pale walipokosa kuelewa.
Wakati tunaondoka nilifuatwa na mwanafunzi wa darasa la saba aliyejitambulisha kwa jina la Saidi Ramadhani aliyetaka kupata maelezo zaidi, na pia kunijulisha kuwa yeye anapenda uandishi na ameshawahi kuandika hadithi kadhaa.
Tutajitahidi kadri ya uwezo wetu kuhakikisha vipaji hivi vipya vya waandishi wa kizazi kijacho, na kubwa zaidi ni kuwafanya wafikirie kuandika zinazoelimisha... ikiwezekana kwenye sayansi na teknolojia.
Mchana tulifika shule ya msingi Kiluvya na kupokelewa na mwalimu Machage ambaye ni mwalimu mkuu, na shughuli yetu ilikwenda vizuri kabisa.
Ushirikiano toka kwa walimu, na hamasa kwa wanafunzi ni vya kuridhisha. Tunatumaini wengi watashiriki.
\Kesho na keshokutwa tutatembelea shule za Makumbusho, Makabe, Muungano, na Mkunguni.
0 comments :
Post a Comment